AhlolBayt News Agency (ABNA)

source : Parstoday
बुधवार

4 अक्तूबर 2023

5:40:44 pm
1397927

Kutomwamini Netanyahu Ben Gvir; mgawanyiko mpya katika baraza la mawaziri la Israel

Gazeti la Yediot Aharonot limeripoti kuwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel hamwaliki tena Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani kwenye vikao vya siri ya juu vya kiusalama vya utawala huo.

Miezi kumi imepita tangu kuanza kazi kwa baraza la mawaziri la muungano la Netanyahu na chama cha mrengo wa kulia cha uzayuni wa kidini. Muungano wa Netanyahu na chama hicho kinachoongozwa na Itmar Ben Gvir unakabiliwa na changamoto nyingi tangu kuanzishwa kwake. Wakosoaji na hata viongozi wa Israel walikuwa wameonya kuhusu kuingia watu wenye misimamo mikali ya kidini kwenye baraza la mawaziri. Hadi sasa, muungano huo umeibua changamoto kubwa kwa utawala ghasibu wa Israel na baraza la mawaziri la Netanyahu.

Changamoto ya kwanza ni kwamba umepelekea kuongezeka migawanyiko ya kisiasa katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Wafuasi wa mrengo wa kulia wa wastani wanaamini kuwa kuwepo serikalini watu wenye misimamo mikali kama  Ben Gvir kunahatarisha nafasi ya mrengo huo katika utawala wa Israel kwa sababu kuwepo kwa shakhsia kama huyo ambaye hana uzoefu wa kisiasa na daima anaibua mivutano, kunahatarisha baraza la mawaziri la Netanyahu. Hii ndio maana baraza la mawaziri la Netanyahu likawa na uungaji mkono mdogo sana kati ya Wazayuni wa Israeli wa mrengo wa kulia.

Changamoto ya pili ni kwamba kuwepo watu wenye itikadi kali kama Ben Gvir kunazidisha pengo kati ya wananchi na baraza la mawaziri. Maandamano ya mara kwa mara ya makumi ya maelfu ya watu katika miezi 10 iliyopita ni moja ya ishara kubwa za kuendelea kupanuka pengo hilo. Kuendelea maandamano na kufikia kileleni pengo hilo kati ya wananchi na baraza la mawaziri kumepelekea hata viongozi wa Israel akiwemo Rais Isaac Herzog kuonya kuhusu kuporomoka kwa ndani na hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya utawala huo.Changamoto ya tatu ni kwamba misimamo mikali ya Ben Gvir na washirika wake katika baraza la mawaziri la Netanyahu imeongeza machafuko kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni, kiasi kwamba sasa Wapalestina wamepata moyo wa kujiunga na harakati na operesheni za mapambano dhidi ya magaidi wa Kizayuni, operesheni ambazo zimeenea hadi ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Tel Aviv. Changamoto ya nne ni kwamba katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, hitilafu za ndani katika baraza la mawaziri zimeanikwa hadharani zaidi. Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani na Yoaf Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wamekuwa na hitilafu kubwa mara kadhaa. Kuhusiana na hilo, Kanali ya 13 ya Televisheni ya Kizayuni imetangaza kuwa katika moja ya vikao vya hivi karibuni vya baraza la mawaziri kuhusu usalama vilivyofanyika katikati ya mwezi Septemba, Ben Gvir alishambulia na kuwakosoa vikali maafisa wa ngazi za juu wa jeshi. Hata hivyo, Yoaf Gallant, Waziri wa Vita, aliwataka maafisa hao wa kijeshi kutomjibu. Kwa kuendelea itikadi kali za Ben Gvir, inaonekana kuwa Netanyahu sasa naye hamwamini tena waziri wake wa usalama wa ndani hivyo ameamua kutomwalika kwenye vikao vyake vya usalama wa juu. Hii ni katika hali ambayo Ben Gvir ni mjumbe wa baraza la mawaziri la usalama la Israel. Gazeti la Aharonot limeandika kwamba Netanyahu kwa kawaida hamwaliki Ben Gvir kwenye vikao hivyo kwa kuhofia kufichuliwa habari na mazungumzo ya siri yanayojadiliwa kwenye vikao hivyo vya siri ya hali ya juu. Hii ni kwa sababu anaamini kwamba Ben Gvir hana wasiwasi wala hofu ya kufichuliwa aina hiyo ya habari za usalama. Kuibuka mivutano na hitilafu za aina hiyo kati ya Netanyahu na Ben Gvir kunaweza kupelekea kuvunjika kwa baraza la mawaziri kwa sababu tathmini ya tabia ya Ben Gvir inaonyesha kuwa si mtu anayetumia busara wala mantiki ya kisiasa hivyo hawezi kuvumilika.

342/